Monday, August 20, 2012

SHERIA ZA TANZANIA DHIDI YA HAKI ZA WATU WAISHIO NA UKIMWI

Sheria zilizopo na inayopendekezwa kwa sasa na serikali ya Tanzania kwa ajili ya kulinda na kusimamia haki za wenye UKIMWI zinatakiwa zilenge au zijikite katika UTAWALA WA SHERIA.Utawala wa sheria hapa namaanisha kusimamia demokrasia katika idara zote, Kuhakikisha uwazi na ukweli katika kutekeleza haki kwa sababu ya usemi usemao(justice should not be done but also should be seen to be done) haki sio tu ifanyike bali pia ionekane ikifanyika, kujiepusha na rushwa, na kuwepo na sheria itakayo kuwa rahisi kutekelezeka na kufanyika.Serikali na viongozi wa siasa wanatakiwa Kuhakikisha haki za watu wenye ukimwi zinalindwa na kuheshimiwa. Uimara, uhuru, na usahihi wa bunge, mahakama, na idara mbalimbali za utawala ni muhimu katika jamii yenye democrasia ya kweli kama vile Tanzania.Sheria ya ukimwi itanufaisha walengwa na wananchi kwa ujumla na kukuza huduma za afya na malengo mengine kama yalivyo tajwa katika Sera ya UKIMWI ya 2001itategemea moja kwa moja etekelezaji wa sheria hiyo.

Mswada wa sheri wa kusimamia haki za msingi za binadamu iliiingizwa katika katiba ya Tanzania mnamo mwaka 1984 na sheria inayolinda haki hizo ni (constitution(fifth)amendment) ACT, 1984 Act no.15 ya mwaka 1984 imetaja mikakati ya kupinga kutengwa kwa watu hawa waishio na UKIMWI katika ibara za katiba yetu hii hasa ibara ya 12 mpaka ya 29.Tutazijadili ibara hizi kwa kina siku nyingine.

Pamoja na hayo, mambo ambayo nitayajadili hapa ni utekelezwaji wa haki hizo zilizopo ndani ya katiba yetu hii,ili zitosheleze kuwalinda watu waishio na UKIMWI ili kuepekana na Kutengwa na kubaguliwa katika jamii na sekta nyingine za umma.

Tanzania, kubagua na kunyanyapaa kunaonekana katika sehemu mbali mbali kama vile, katika ngazi ya familia, vyombo vya habari, sehemu za kazi, idara ya elimu, idara ya afya, na dini pia. Unyanyapaa na kubagua dhidi ya watu waishio na UKIMWI kunasababisha jitihada za kuzuia na kupambana na UKIMWI kuwa ngumu.

Nchini hapa(Tanzania) kuna zana na njia mbalimbali za kisheria ambazo zipo kwa ajili ya kulinda uvunjaji wa haki za binadamu zilizo hakikishwa ndani ya katiba ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Miongoni mwa njia zitumikazo ni bunge kubadili sheria mbalimbali kwa mfano;

Sheria ya mashtaka dhidi ya serikali(government proceeding Act) 1967 ambayo kabla ilikuwa ikimtaka mtu kupata idhini ya mwanasheria mkuu ili aishitaki serikali hata kama imefanya kosa kubwa kabisa la uvunjaji wa haki za binadamu.Baada ya kubadilishwa sasa mtu anaweza kuishtaki serikali baada tu ya kuitumia notisi ya siku 90 kuonyesha dhamira yake ya kutaka kuishtaki.Sheria nyingine ni ( BASIC RIGHTS AND DUTIES ENFORCEMENT ACT NO.33 1994)

Sheria hii ya utekelezaji wa haki na wajibu ya mwaka 1994(BASIC RIGHTS AND ENFORCEMENT ACT 1994), ni sheria itoayo utaratibu wa utekelezaji wa haki za msingi zilizotolewa ndani ya katiba na mambo mengine kama hayo. Kwa hiyo mtu yeyote ambae anadai kuwa moja wapo ya ibara ya 12 mpaka 29 ya katiba imevunjwa au inaelekea kuvunjwa anaweza kuomba au kufungua mashtaka mahakama kuu ya Tanzania kw ajili ya kupata haki zake. Hii ni kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha sheria hii.

Kifungu cha 13 cha sheria hii, kinasema pamoja na mambo mengine kama mahakama kuu itaona kuwa ni kweli haki za mtu huyo zimevunjwa itakuwa na nguvu ya kuamuru haki hizo kutekelezwa juu ya mtu huyo kama zilivyo tolewa katika ibara ya 12 mpaka ya 29.

PAMOJA NA HAYO, Utekelezwaji na usimamizi wa vifungu hivi katika sheria hii haupo kivitendo. Hii ni kwa sababu zifuatazo:

Kwanza, sheria hii ndani yake kuna ibara ya 10 ambayo inasema katika utoaji wa haki hizi panatakiwa kuwepo na majaji watatu kusikiliza madai hayo badala ya jaji mmoja.
Kwa Tanzania ni vigumu kuwa na majaji watatu katika kikao kimoja kwa sababu ya ukosefu wa majaji nchini kwetu, hiki ni kipingamizi kwa kuwa watu huona kesi zao zitachukua mlolongo mrefu mahakamani katika kusubiri hadi majaji watatu wakae.

Kwa kifupi kifungu cha 10 na 13 cha sheria hii ya mwaka 1994 kinatakiwa kitazamwe upya kama kweli tunataka kupambana na ugonjwa huu na haki za watu hawa kwa ujumla kwa kuwa vifungu hivi kwa ujumla wake havitoi nafasi kwa watu waishio na ukimwi kuzipata haki zao za msingi.

NITAENDELEA KUZIJADILI SHERIA NYINGINE ZINAZO ONYESHA UWEZEKANO WA KUWABAGUWA NA KUWANYANYAPAA WENYE UKIMWI.

No comments: