Sunday, 12 August 2012 00:21
UGONJWA wa Ukimwi hautakuwa tena janga la kitaifa nchini miaka michache ijayo baada ya Tume ya Taifa ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) kueleza kuwa Tanzania imekusudia kubadili sera na mikakati ya kukabili ugonjwa huo.
Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa Tacaids, Dk Raphael Kalinga aliliambia gazeti hili jijini Dar es Salaam mapema wiki hii kuwa, chini ya mkakati huo Ukimwi utakuwa ni tatizo la mtu binafsi na makundi maalumu.
Mpango huo unafuatia matokeo ya Mkutano wa Kimataifa wa Ukimwi uliofanyika nchini Marekani hivi karibuni na kujifunza juu ya maendeleo ya kisayansi ya kudhibiti Ukimwi ambao ujumbe wa Tacaids ulihudhuria akiwamo Dk Kalinga.
"Awali tulikuwa tunakubaliana kuwa, ‘Ukimwi ni janga la Kitaifa’. Kwa maana kwamba tulikuwa tunaenda na population yote (idadi ya watu nchi nzima)," alisema Dk Kalinga kwenye mahojiano na Mwananchi Jumapili mapema wiki hii, baada ya kurejea nchini kutoka Marekani.
Alisema kuwa, sera hiyo ya kizamani na kwamba sasa wataachana nayo na inawapasa kubadilika kulingana na tafiti za kisayansi, maendeleo na uzoefu uliothibitishwa kitaalamu.
Dk Kalinga alisema kuwa, mkakati ambao Tanzania itautumia ni wa kuuona Ukimwi kama janga la mtu binafsi na makundi maalumu yaliyo kwenye mazingira hatarishi.
"Kwa kutumia mbinu zenye kuleta matunda mazuri, tumeingia kwenye ubunifu mpya. Hatuutazami tena (Ukimwi) kama janga la kitaifa. Tunalitazama kama ni janga langu, au janga lako," alisema Dk Kalinga na kuainisha:
“Mtazamo wa Tacaids sasa ni kujikita zaidi kwenye makundi ya watu maalumu walio kwenye mazingira hatarishi, kama vile wanaofanya kazi migodini, wafungwa, wanaoendesha biashara ya kuuza miili yao na watumia dawa za kulevya.”
Dk Kalinga alisema kuwa, tatizo la Virusi Vya Ukimwi (VVU) ni la mtu binafsi.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa, kila mtu anapaswa kufahamu kwamba Ukimwi ni tatizo hadi hapo itakapopatikana dawa ya chanjo au tiba iliyothibitishwa na mamlaka zinazotambulika duniani.
Dk Kalinga alibainisha kuwa, pamoja na kuwapo na dawa zinazozuia maambukizo, hata kutumika kama tiba, bado kila mtu atapaswa kuendelea kutumia elimu ya kukabiliana na VVU.
Alifahamisha elimu hiyo kuwa, ni pamoja na matumizi ya kondomu, wanaume kutahiriwa, kutibu mapema magonjwa ya zinaa, kuwa na mazoea ya kupima na kujua hali ya kiafya, kuzuia maambukizo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, ushauri nasaha, damu salama na matumizi sahihi ya dawa za kupunguza makali ya VVU (ARV).
Dk Kalinga alisema pia kwamba wanatarajia kufanya kikao kitakachojumuisha wataalamu wa afya, watunga sera na wadau wa mapambano ya VVU nchini.
Kuhusu mkutano wa kukabiliana na Ukimwi uliofanyika Washington alisema kuwa, kimsingi katika mkutano huo uliomalizika Julai 27, mwaka huu waliazimia mkakati wa kuhakikisha kuwa hakuna unyanyapaa, kufa, kuambukiza ya VVU.
"Mkakati wetu ni kuwa na unyanyapaa sifuri, vifo sifuri na maambukizo sifuri," alisema Dk Kalinga ambaye pia ni mmoja wa wataalamu wa utafiti wa magonjwa ya binadamu nchini.
Mkutano huo ulikuwa wa kwanza kutamka kuwa VVU vinaweza kuangamizwa kabisa duniani.
Chini ya kauli ya kutokuwa na dawa wala chanjo, mkutano huo umeufumbua macho ulimwengu kwa kueleza kuwa zipo dawa zinazozuia mtu kuambukizwa Ukimwi, kuambukiza na kutibu.
Alipoulizwa nafasi ya Tanzania kufaidika na maendeleo hayo, Dk kalinga alisema pamoja na maendeleo hayo, nchi tajiri zina nafasi kubwa ya kufaidika zaidi zikilinganishwa na nchi maskini kama Tanzania.
Alisema katika nchi zilizoendelea, kama Marekani, watu wake wako katika nafasi nzuri zaidi ya kutumia dawa maalumu zinazozuia kuambukizwa VVU kutokana na mazingira yake ya elimu, ubora wa huduma za afya, uwezo wa kifedha na urahisi wa mawasiliano.
Hata hivyo, Dk Kalinga alibainisha kuwa hatari ya dawa hiyo kutumika katika nchi maskini kuwa ni kusababisha usugu wa maradhi hayo kwa sababu watu ambao hawajajichunguza kikamilifu kama wameambukizwa VVU wanaweza kuitumia.
Alisema kitaalamu dawa hiyo inapaswa kutumiwa na mtu asiye kabisa na virusi mwilini.
Hata hivyo, alisema kwa mazingira ya nchi maskini, ARV zina nafasi ya kusaidia kuzuia maambukizo ya Ukimwi, hata kutibu na kumfanya mwathirika aweze kuishi bila matatizo makubwa ya kiafya.
"Dawa za kuzuia kuambukizwa zikiletwa hapa wengi wataanza kuzitumia bila kujua hali zao kama wameambukizwa. Tuna uzoefu wa watu wetu, wanaweza wakadharau kwenda kupima na kusema: 'acha tu nimeze, itajulikana tu huku mbele', jambo ambali kiafya ni hatari," alionya Dk Kalinga.
Alisema mkutano huo kuhusu Ukimwi uliomalizika nchini Marekani umekuwa ukifanyika kila baada ya miaka miwili kwa kuwakutanisha wanasayansi, watunga sera na wadau wa mapambano ya VVU kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu mpya na kuoana namna bora ya kupata fedha za kukabili tatizo hilo dunia nzima.
Maazimio ya mkutano
Jumamosi iliyopita, gazeti la Mwananchi liliripoti kuhusu mkutano huo uliomalizika kwa wajumbe zaidi ya 20,000 kuridhia maendeleo ya kisayansi yaliyofikiwa kwa sasa, wakisema ni madhubuti hivyo kutoa azimio la kuungana kuangamiza janga la maradhi hayo duniani.
Moja ya maazimio yao ni kuifikisha dunia mahali ambapo hakutakuwa na mtu atakayekufa, wala atakayekuwa akiishi na VVU.
Hii inatokana na matumaini ya kisayansi waliyohakikishiwa na watafiti juu ya kuwepo kwa dawa zinazoweza kuzuia maambukizo mapya na ambazo zikitumika kikamilifu zinaweza kufanya kazi kama tiba.
Pamoja na kuwapo kwa dawa hizo, walikiri kuwa mkakati huo hauwezi kufikiwa iwapo dunia haitajenga mshikamano wa pamoja wa kisera, uelimishaji na fedha za kutosha kufanikisha mbinu hizo mpya za kisayansi.
Rais wa Taasisi ya Kijamii ya Kimataifa ya Mapambano dhidi ya VVU (IAS), Dk Elly Katabira alisema kuna mambo mengi yaliyothibitishwa kisayansi huko nyuma, lakini kwa kuwa hakukuwa na mikakati madhubuti, tatizo hilo limeendelea kuwa janga la dunia.
Dk Katabira ambaye pia ni mmoja wa watafiti wa kisayansi katika Chuo Kikuu cha Tiba cha Makerere, Uganda alitoa mfano wa watoto kuendelea kuambukizwa Ukimwi wanapozaliwa wakati tayari dawa ya kuondoa tatizo hilo ipo.